KIKWETE ATUNUKIWA TUZO YA UONGOZI WA KISIASA NA UTETEZI
Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akipokea
Tuzo ya Uongozi wa Kisiasa na Utetezi
kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Speak Up Afrika Bi Kate Campana,
hafla iliyofanyika Alhamis jana ,
New York Marekani
Na
Mwandishi Maalum, New York
Shirika lisilo la
Kiserikali la Speak Up for Afrika
limemtunukia tuzo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na
uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake kwa makundi ya jamii yaliyo
katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.
Utoaji wa Tuzo hiyo
ya uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba
na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa kwa Taasisi ya
Speak up Afrika. Hafla hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New
York ilikuwa pia ni sehemu ya kuhamasisha
uchangiaji wa shughuli za Taasisi hiyo.
Mchango ambao umetambuliwa
na Speak Up Afrika, taasisi ambayo imekuwa ikifanya
kazi kwa Karibu na Rais Mstaafu Kikwete, ni katika maeneo ya
upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na
mtoto, udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia kampeni
ya malaria haikubaliki ,usambazaji wa vyandarua vyenye viatilifu, kampeni
ya lishe bora, na kampeni ya chanjo kwa watoto.
Pamoja na
kutambua juhudi za Rais Mstaafu Kikwete katika
kuyasemea maeneo hayo, Taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi wake
Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua kama kiongozi
ambaye amekuwa mstari wa mbele wa kulisema Bara la
Afrika kila mara alipopata fursa ya kufanya hivyo
wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
Rais kikwete ameelezwa
katika hafla hiyo iliyowashirikisha wadau wa kada mbalimbali, kama
kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwaajili ya
watu wenye mahitajio ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo au
wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.
Akipokea Tuzo hiyo,
Rais Mstaafu Kikwete , amesema Tuzo hiyo ni ya watoto wote waafrika
ambao ndio waliomfanya asimame mbele ya wageni waalikwa.
“ Ni kwa sababu yenu ndio
sababu nimetenga muda wangu baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda
ya kuboresha maisha yanu. Ninafanya hivyo kwasababu makuzi yangu yalikuwa
kama ya mtoto yeyote yule wa kiafrika, nimeyaishi maisha
wanayo ishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika hamu na kiu yao ya kuwa na
maisha bora na afya njema”. Akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.
Akaongeza kuwa
, mafaniko ambayo ameyapata katika juhudi hizo za
kufikisha huduma za msingi za kijamii kwa makundi yenye mahitaji
yametokana na mambo mawili makubwa moja ni aina ya uongozi
alioutumia kusukuma harakati hizo. Na pili uhamasishaji uliofanyika
katika kupiga vita malaria kupitia Speak Up Afrika na
kampeni yao ya malaria haikubaliki.
“ Nisingeweza kuyafanya
niliyoyafanya bila uungugwaji mkono na ushirikiano wa
karibu nilioupata na ninaoupata kutoka taasisi za kimataifa ikiwamo
hii ya Speak Up Afrika. Ndio maana kwa mfano, tumeweza
kupunguza visa vya malaria kwa theluthi mbilli,
tumefanikisha upatikanaji wa chanjo kwa asilimia 96 kwa watoto wote na
kupunguza vifo vitokanavyo na malaria kwa nusu.” Akaeleza
Kikwete na kushangiliwa tena.
Akasema, anamini katika
ushirikiano na wadau mbalimbali kama akina Ray Chambers kupitia kampeni
ya hakuna tena malaria, Taasisi ya Bili na Melinda Gates na Gavi
Vaccination Alliance ambayo anashirikiano nayo kwa karibu
katika kampeni ya chanjo kwa wote.
Rais Mstaafu
amewahakikishia watendaji wa Speak Up Afrika kwamba
ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu kutokana kile alichosema
amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifana.
Akawasihi wadau
mbalimbali kuichangia taasisi hiyo kwa kile alichosema, inafanya
kazi kubwa ya siyo tu kufikisha huduma za kijamii pale zinapotakiwa
lakini pia imekuwa ni kipaza sauti cha Afrika.
Wengine waliopewa Tuzo kwa
kutambua michango yao kwa jamii ni pamoja na Professa Awa
Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya wa Senegal, Bibi Toyin
Saraki, mwanzilishi wa Taasisi ya Wellbeing Afrika
ambayo pia imekuwa ikitoa elimu na misaada kwa wanawake na watoto
pamoja na elimu kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu
ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua. Na Bwana Kabirou
Mbodje ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Wari.
Taasisi ya
Speak Up Afrika imeanzishwa na wanawake na inaongozwa
na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uweo na sifa kubwa ndani ya
kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.
Posted by Elias Magugudi
0 comments:
Post a Comment