Laws and regulations, politics and democracy in general

Vertical Sample

Sunday, July 31, 2016

KANUNI NAMBA 7(3) YA KANUNI ZA UPIMAJI WA MAGARI KWENYE MIZANI ITEKELEZWE




Kanuni 7(3) ya Kanuni za Usalama Barabarani kuhusiana na Ukomo wa Uzito wa Juu wa Magari za Mwaka 2001
*Na. Elias Magugudi

Utangulizi
Madhumuni ya maada hii ni kujadili tatizo la utekelezaji wa kanuni namba 7 (3) ya Kanuni za Usalama Barabarani kuhusiana n Ukomo wa Uzito wa Juu wa Magari za Mwaka 2001.
Tanzania ilitunga sheria ya Usalama Barabarani tangu mwaka 1973 kwa lengo la kudhibiti uzito wa magari barabarani. Sababu ya kutunga sheria hii ilikuja baada ya kuona uzito wa magari kwenye ekseli ukizidi ule uliokadiriwa wakati wa usanifu wa barabara husababisha barabara kuharibika kabla ya muda wake uliotegemewa. Uharibufu huu unaleata hasara kwa Serikali ni kwa sababu hii ndiyo maana sheria ya Usalama Barabarani Na.30 ya mwaka 1973 na kanuni zake zinawekewa mkazo na Serikali. Hata hivyo baadhi ya kanuni hizo zimekua zikileta mgogoro mkubwa kati ya serikali na wasafirishaji hadi kusababisha sheria hizo kutotekelezwa. Mgogoro kubwa baina ya wasafirishaji na serikali upo katika utekelezaji wa kanuni namba 7(3).
Sheria na Kanuni zinazotumika Tanzania
Duniani kote kuna sheria na kanuni mahsisi zinazosimamia viwango vya uzito wa magari kwa lengo la kulinda barabara zisiharibike kutokana na uzito wa magari yanayopita katiba barabara hizo. Kanuni hizo zimeainisha aina za magari na viwanga vya uzito wa jumla wa gari (Gross Vehicle Mass).[1]

 Kanuni hizi pia zimeainisha viwango vya uzito unaopaswa kubebwa na axle zinazobeba mzigo hadi kwenye matairi ya gari.

Kanuni za Usalama Brabarani (Uzito wa Juu wa Magari) za mwaka 2001 au The Road Traffic( Maximum Weight of Vehicles) Regulation, 2001 ndio sheria inayotumika sasa katika upimaji wa magari. Kanunu hizi zimetungwa chini ya kifungu 114 (1) (p) cha sherai ya usalama barabrani, namba 30 ya mwaka 1973[2]
Tatizo la kubwa katika utekelezaji wa sheria na kanuni zake liko katika kanuni 7 (3) ya Kanuni za Usalama Barabarani za mwaka 2001. Kanuni hii inaelekeza kwamba, mzigo uliozidi lakini upo ndani ya asilimia tano (5%) tajwa, lazima upangwe upya ili kila ekseli iwe na uzito unaoruhusiwa la sivyo mzigo utapakuliwa , la kama mzigo huo haupangiki na hautapakuliwa  na hivyo lazima ubebwe ulivyo, basi ada ya ziada (surcharge fee) ya mara nne ya ile ya kawaida lazima ilipwe. Kanuni hii ndio inayolalamikiwa na wasafirishaji kutokana na madai , masharti yake ni magumu na hayatekelezeki  kwa kuwa ni mzigo kwao.

Madhumuni ya Kanuni namba 7 (3)

Mzigo uliopakiwa kwenye gari unaweza kusogea wakati wa safari , mfano mzigo unaweza kusogea kwenda mbele wakati wa kuteremka mlima au kusimama ghafla kwenye tuta. Kanuni namba 7(3) inatoa nafasi kama mzigo umesogea ekseli ikawa na mzigo mzito kuliko kiwango kilichoruhusiwa yaani ndani ya asilimia tano, mmiliki wa gari atapaswa kupanga upya au kushusha mzigo uliozidi . Kama itashindikana kupanga au kushusha mzigo uliozidi gari husika litaruhusiwa kuendelea na safari lakini kwa kulipishwa mara nne ya faini ya kawaida. Hata hivyo iwapo mzigo utapangwa na kuonekana kutozidi uzito unaoruhusiwa kwenye ekseli zake gari litaruhusiwa kuendelea na safari bila kulipishwa chochote.

Chanzo cha Mgogoro
Tarehe 01 October 2013 Wizara ya Ujenzi ilitoa Taarifa kwa Umma kwamba kuanzia tarehe o1.October, 2013 magari yote yenye uwezo wa kubeba tani 3.5 na kuendelea yatakuwa yanapimwa bila msamaha wa tozo uliozidi (overload) ndani ya asilimia 5% ya uzito unaokubaliwa kisheria.[3]

Tangazo hilo lilikua linafuta mwongozo uliotolewa na Waziri mwenye dhamana ya Miundombinu uliotolewa mwaka 2006 [4]ambao ulitoa msamaha wa tozo kwa magari uliozodi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria. Katika tangazo hilo la Wizara ya Ujenzi wasafirishaji wa magari yenye uzito wa tani 3.5 na kuendelea walitakiwa kuzingatia utaratibu ulioainishwa katika sheria.[5]Baada ya kutengua mwongozo uliotoa msamaha, magari yote yatakayobainika kuwa na uzito uliozidi lakini upo ndani ya asilimia tano (5%) ya uzito unaokubaliwa kisheria yalitakiwa kupunguza mzigo, kupanga mzigo au kulipia mara nne ya tozo ya kawaida.[6]

Changamoto za Ukiukwaji wa Kanuni namba 7 (3)

Uzito wa Serikali katika kutekeleza sheria na kanuni kama ilivyoainisha katika kanuni umekua ukisababisha magari yenye uziti mkubwa kuendelea kutembea katika barabara zetu. Katika takwimu za Wakala Barabara nchini Tanroads za mwaka 2011/2012, jumla ya magari 684,600 yalipimwa katika mizani , magari 167,310 ambayo ni sawa na asilimia 24.44% alionekana kuwa yamebeba mzigo uliozidi kwa mujibu wa kanuni. Magari 8,856  ambayo ni sawa na asilimia 1.30% yalikua yamezidisha uzito juu ya asilimia tano. Ripoti inaonyesha kwamba asilimia 98.7% ya ulizo uliozidi katika mwaka huo ilikua ndani ya asilimia 5%.[7]

Katika mwaka 2013/2014 jumla ya magari 3,060,057 yalipimwa katika mizani, kati ya magari hayo, 790,777 ambayo ni sawa na asilimia 2.84% yalikua yamezidisha uzito. Asilimia 1.62% tu ya magari yaliyopimwa katika mwaka huo ndiyo yalikuwa yamezidisha uzito nje ya asilimia 5%.[8]

Kwa kuwa barabara zetu zimesanifiwa ili ziweze kudumu kwa miaka kumi na tano hadi ishirini, ni ukweli usiokuwa na kificho kwamba barabara haziwezi kudumu kwa umri uliokadiriwa kwa sababu magari yanaendelea kutembea na uzito uliozidi ule unaotakiwa kisheria japokuwa upo ndani ya asilimia tano.[9]

Hitimisho
 Mwaka 2006 Waziri mwenye dhamana ya Miundombinu wakati huo, alitoa msamaha wa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano (5%) ya uzito unaokubaliwa kisheria kwa lengo la kutafuta suluhu ya malalamiko ya Wasfirishaji yaliyoletwa kwake ambayo yalisababishwa na ubove wa barabara, matuta na mapungufu katiaka mizani za kupimia uzito. Kanuni na misingi inayojulikana kisheria ni kwamba, Sheria ya kanuni haiwezi kufutwa kwa barua hata kama imetoka katika Mamlaka husika. Pamoja na kwamba mheshimiwa waziri alitoa maelekezo kupitia barua bado kanuni zinanaelendelea kuwa vilevile japokuwa hazitumiki.
 Waziri mwenye dhamana ya Ujenzi aliamua kufuta muongozo huo ili kanuni ziweze kutekelezwa kama zilivyotolewa mwaka 2001.Inawezekana kanuni hio imeonekana kuwa na masharti magumu kwa wasafirishaji na kuleta malalamiko kwa sababu kanuni hazijatumika kwa muda mrefu.  Ni matumaini yangu kwamba pamoja na mambo mengine Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi iliamua kufuta muongozo uliotolewa mwaka 2006 baada ya kuridhika na maendeleo yaliopatikana  katika sekta ya Ujenzi ikiwa ni pamoja na barabara na mizani. Kwa vile changamoto zilizokuwepo mwaka 2006 zimekwisha au kupungua kwakiasi ni kikubwa imefika wakati sasa Kanuni zilizopo zitumike kama zilivyo.


 *Shahada ya Sheria (LLB), Chuo Kikuu Mzumbe, Pia nipo katika masomo ya Shahada ya Pili ya Sheria (Masters in Law by Thesis), Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania
[1]  Hotuba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

[2] Manual for Weighbridge Operators,Tanroads
[3] Hotuba ya Waziri Mkuu  Mizengo Pinda (sasa Waziri Mkuu mstaafu)  wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo vya Habari  kuhusu suala la wasafirishaji wa maroli na mabasi kuondolewa nafuu ya kutolipa tozo kwa  wa Magri uliozidi (overload) ndani ya 5% ya uzito unaokubaliwa kisheria , Katika Ukumbi wa Waziri Mkuu Dar es salam October 10, 2013
[4] Mwongozo ulitolewa kupitia barua yenye kumb. Na.CKA/16/419/01 ya tarehe 19 Julai 2006
[5] The Road Traffic Act Cap 168 R.E 2002 pamoja na kanuni zake, The Road Traffic ( Maximum Weight of Vehicles) Regulations, 2001
[6] Hii ni kwa mujibu wa Kanuni ilivya hadi leo, aangalia Kanuni namba 7 (3) ya Kanunu za Usalama Barabarani Kuhusiana na Ukomo wa Uzito  wa Magari za mwaka 2001.
[7] Msuya E.( January 18,2014) “Pinda Kuitia Hasara Serikali” Mwananchi or www.tanroads.go.tz
[8] ibid
[9] Zimetumika rekodi za miaka ya nyuma kwa sababu ndizi zilizoweza kupatikana kwa haraka..









































0 comments:

Post a Comment